Tarehe 16 Machi 2013 nitaongoza maandamano ya amani ya wananchi kwenda
kwa Waziri wa Maji kusimamia uwajibikaji kuwezesha hatua za haraka za
kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka katika
Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam.
Wote mlioshiriki mkutano wa tarehe 10 Februari 2013 (Kwa wale ambao hamkushiriki mnaweza kutazama video hii: YOUTUBE , mtakumbuka tulimpa wiki mbili Waziri kujitokeza kwa wananchi kujibu hoja alizokwepa kujibu bungeni.
Tutakusanyika
kata ya Manzese eneo la Bakhresa (jirani na daraja) saa 5 asubuhi na
tutapita barabara ya Morogoro kuelekea kata ya Ubungo zilipo ofisi za
Wizara ya Maji kufuatilia majibu ya ukweli na ukamilifu kuhusu hatua
tisa za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa
majitaka nilizopendekeza kwa niaba ya wananchi bungeni kupitia hoja
binafsi na masuala mengine ambayo wananchi watataka yatolewe majibu siku
hiyo.
Kila mmoja anaweza kuendelea na maandalizi ya kushiriki
kwa kuwa tayari tarehe 4 Machi 2013 nimewasilisha notisi kwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni na Maafisa wa Polisi Wasimamizi wa Maeneo kwa
kuzingatia masharti ya kifungu cha 43 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na
Huduma Saidizi Sura ya 322 (The Police Force and Auxiliary Service Act,
Chapter 322).
Itakumbukwa kwamba baada ya kutoa wiki mbili
Waziri alijitokeza mara tatu ndani ya wiki hizo; mbili kati ya hizo
ikiwa ni kupitia mikutano ya CCM na mara moja ikiwa ni kwenye mkutano
kati yake na wafanyakazi wa DAWASA na DAWASCO.
Katika mkutano wa
hadhara wa CCM uliofanyika Temeke mwisho tarehe 16 Februari 2013,
Waziri hakutoa majibu badala yake alirudia tena maelezo yale yale potofu
aliyoyatoa bungeni tarehe 4 Februari 2013.
Kwenye mkutano wa
hadhara wa Goba tarehe 17 Februari 2013 ambapo aliahidi maji kutoka
tarehe 20 Februari, 2013 ambayo hayakutoka. Tarehe 23 Februari 2013
nilifanya mkutano Goba na kutangaza namba zake za simu wananchi wamhoji
ahadi hiyo na kutaka Manispaa, DAWASA na DAWASCO waweke kambi Goba mpaka
maji yatoke.
Shinikizo hilo limesaidia baadhi ya maeneo ya Goba
maji yameanza kutoka hata hivyo maeneo mengi bado hali ambayo inahitaji
hatua za haraka nilizopendekeza bungeni kuhusu kata hiyo ziweze
kutekelezwa.
Kupitia mkutano wake na DAWASA na DAWASCO tarehe 21
Februari 2013 (tofauti na maelezo yake bungeni) alikiri kwamba kuna
upotevu wa maji ikiwemo kwa wizi, kuna biashara haramu yenye kuhusisha
hujuma ya miundombinu, bei ya juu ya maji na kutozingatiwa kwa ratiba ya
mgawo wa maji katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.
Hata
hivyo, zaidi ya wiki moja imepita Waziri wa Maji na Wizara kwa ujumla
haionyeshi kwa matendo kuisimamia kwa karibu EWURA, DAWASA, DAWASCO na
Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka ambazo nilizieleza kwenye
hoja binafsi.
Hivyo, wote mlioahidi kupitia mkutano wa tarehe
10 Februari 2013 kushiriki maandamano na wote ambapo mnaguswa na
matatizo ya maji katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo na Jiji la
Dar Es salaam tukusanyike Manzese tarehe 16 Machi 2013 saa 5 asubuhi
tuandamane kwenda Wizara ya Maji kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara za
8, 18, 20 na 21.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
05/03/2013
No comments:
Post a Comment