UDINI NA TANZANIA: TULIPOTOKA,TULIPO NA TUELEKEAPO


MCHANGO WA MOBHARE MATINYI KATIKA MJADALA WA UDINI

Naomba nichangie hapa kama Mtanzania - na si kama mwislamu au mkristo au mpagani.

1. Kwanza ni kweli kwamba kitabu cha yule padri mzungu kinaleta shida sana mawazoni mwa watu, Dkt. Sivalon. Lakini turejee kwenye ukweli wa kisomi, kwamba huwezi kuhitimisha jambo zito kwa kutumia chanzo kimoja. Hatuna maandiko mengine ya watu wasiokuwa na upande yanayothibitisha aliyosema bwana huyu. Hakuna utafiti wowote. Aidha, ni muhimu pia kuchunguza kujua alisema hivyo katika mazingira gani. Kuna Mkenya mmoja London aliwahi kuzuliwa na wenzake kwamba ni shoga na akatengwa kabisa. Aliyemzulia siku moja akamwambia Mkenya mwingine ninayemfahamu, kwamba anajua fika kuwa bwana yule si shoga lakini alifanya vile kumlipizia kisasi cha ugomvi wao. Uongo ulibadilishwa kuwa ukweli. Je, tuna hakika na maneno ya huyu mwandishi padri? Najua ukivutia upande mmoja itabidi useme uhakika upo kwa sababu kuna uthibitisho mwingine, lakini hali halisi inagoma. Nitaeleza.

2. Pili, ingawa Mwalimu Julius Nyerere analaumiwa sana na waislamu au watetezi wa waislamu, lakini kiukweli kama si yeye, hali ya kielimu ya waislamu nchini ingekuwa mbaya sana. Tusisahau kuwa, tulipopata uhuru serikali ya Mwingereza hakituachia shule za kutosha. Wakristo na dini za Waasia wakiwemo Wabohora, Waismailia na Wahindu walikuwa na shule lakini Waislamu hawakuwa na shule. Sasa ukumbuke pia kuwa, wakoloni wa Ulaya walikuja Afrika Mashariki kwenye karne ya 19 wakati wakoloni wa Uarabuni walikuwa tangu karne ya 13. Kwa miaka 600 Waarabu hawakujenga shule hata moja; bali walijenga madrasa kwa ajili ya masomo ya dini - jambo ambalo halikuwa dhambi. Shule za kwanza zilijengwa Tanganyika na Mjerumani zikiwa ni za darasa la kwanza hadi la nne kwa kutumia Kiswahili. Zanzibar zilijengwa sana sana na Mwingereza. Tafuta maana na historia ya maneno haya: (i) Darasa/Madarasa (ii) Shule (iii) Skuli. Kimsingi, Nyerere ndiye aliyezitaifisha shule za wasiokuwa waislamu ili na watoto wa waislamu waende kusoma kwa sababu walikuwa wanakwepa kubadilishwa dini na kulishwa nguruwe ingawa wakristo wengine kama wasabato hawali nguruwe.


3. Nchi yetu ikapiga hatua zaidi na tukaanza kujenga shule za msingi. Nyerere akajenga shule kwa juhudi kubwa zaidi kwenye mikoa iliyokuwa nyuma, ambayo mingi ilikuwa ni ya pwani waliko waislamu wengi zaidi. Haikutosha, baada ya Nyerere kuibana mikoa mingine, ambayo wananchi wake waliamua kujijengea wenyewe, akaweka nafasi maalum kwa watu wa makabila ambayo hayakuwa na watoto wengi shuleni, yaani hayakuwa yanataka shule. Waliofaidika zaidi ni makabila ya pwani ambako shule ilikuwa kama kituo cha polisi kwao. Dini yao wengi wao tunaijua. Mwalimu akiwa anaongoza TANU na CCM akajenga shule za jumuiya ya wazazi kwenye mikoa ya pwani na hata alipopata msaada kutoka Kuba (Cuba), aliichagua mikoa ya pwani pia kujengewa shule, na ndipo tukapata shule kama Kibiti, Ruvu, n.k. Hata ile ya Waswidi ilijengwa Kibaha. Alifanya hivi kuwasaidia hao mnaowaita waislamu (mimi nawaita Watanzania). Kule kwingine kama Kilimanjaro, wakaamua kujenga shule za binafsi zao wenyewe na ndio maana hadi leo wanazo nyingi. Serikali ya Nyerere haikujenga shule za sekondari kule bali ilijenga hizo chache kwenye mikoa yenye waislamu wengi. Ndio ukweli huo ila watu hawataki kuutafuta. Rekodi zipo, tafuta shule zote uone.

4. Serikali ya Tanzania haikuishia hapo. Wakati wa Rais Mwinyi waislamu wakiongozwa na Waziri Kighoma Malima walilalamika sana. Zikafanyika juhudi nyingi ikiwemo kumweka Malima kwenye sehemu kama elimu ambapo alianzisha awamu mbili za kwenda shule, lengo likiwa kuongeza idadi ya watoto wa kiislamu wanaoingia sekondari ingawa na wakristo pia waliongezeka. Pia Tanzania ikapata nafasi za masomo kwenye mataifa ya Misri, Algeria, Iran, na Uturuki, maalum kwa ajili ya waislamu tu. Marafiki zangu walikwenda huko na walinithibitishia kwamba hii ilikuwa maalum kwa waislamu tu. Bado waislamu waliendelea kwenda nchi zingine zisizokuwa za kiislamu bila tatizo. Huu ulikuwa msaada mkubwa.

5. Ikaja serikali ya Ben Mkapa na yenyewe ikaweka rekodi ya kuipa dini moja majengo ya chuo kikuu. Leo hii kipo chuo kikuu cha waislamu Morogoro kwa kutumia majengo ya serikali. Serikali ya JK imejenga shule nyingi sana za sekondari nchi nzima na sijasikia ubaguzi kwa upande wa mikoa yenye waislamu wengi. JK pia amehakikisha waislamu wanaongoza wizara ya elimu ili kuondoa malalamiko, na si kweli kwamba eti asiyekuwa mwislamu akiwa waziri wa elimu, basi waislamu wanashindwa kusoma. Hakuna ukweli hapa.

6. Najua kuna malalamiko mengi kuhusu shule na hata hospitali za misheni, lakini tuzitendee haki. Hizi ni za kuhudumia Watanzania wote, na ndiko Kikwete na binti yake waliposoma, hata Mzee Makamba. Tuweni wakweli kwenye hili. Waislamu wanatibiwa kote huku, na ruzuku ndiyo mkombozi wa Mtanzania mnyonge.

WAISLAMU KWENYE VYEO NA ELIMU

7. Labda, tuje kwenye hili moja: KWA NINI HATUNA WAISLAMU WENGI KATIKA NAFASI ZA JUU SERIKALINI? Hili jambo ni la kweli lakini inabidi tujiulize swali jingine zaidi: KWA NINI KUNA MADAI KWAMBA WAISLAMU HAWAJASOMA?

8. Nianze na historia yetu. Waarabu walipokuja kwenye karne ya 13 walileta vitu kadhaa vikuu vikiwa ni dini nzuri ya Kiislamu na pili utamaduni wao wa kishenzi. Ndiyo, walileta utamaduni wa kishenzi. Utamaduni wa Kiarabu siyo dini ya Kiislamu na dini ya Kiislamu siyo utamaduni wa Kiarabu. Uislamu ndio ulioongoza elimu duniani kwenye karne ya saba na nane na hata vyuo vikuu vya kwanza duniani vilikuwa vya Waislamu, lakini si Waislamu wote hupenda elimu, kama ilivyo kwa dini zote zingine pia. Ukienda kwenye nchi za Maghrebu na baadhi ya Mashariki ya Kati, yaani Moroko, Algeria, Tunisia, Misri na zile za Uturuki, Siria, Iraki na Yodani, kuna waislamu wengi wenye elimu. Hapa Marekani wanaheshimika, mathalani, wahandisi mahiri hutoka Uturuki, Pakistan na India kwenye majimbo yenye waislamu.

9. Hali ni tofauti kabisa kule Ghuba kwenye nchi za Saudia Arabia, Yemeni, Kuwaiti, Omani, Katari, Imarata na Bahraini. Ghuba watu hawataki shule. Hawa wa Ghuba ndio walioletea ushenzi wao huu Afrika Mashariki kuanzia kule Somalia hadi Msumbiji kaskazini - kote huku kuna watu wenye utamaduni wa Ghuba wa kukataa shule. Hili liko wazi. Kwa kuwa Waarabu wa Ghuba ndio walioleta pia Uislamu, basi watu hujumuisha kwa pamoja tatizo la kukosa elimu kwa sababu za kuiga utamaduni wa Ghuba na dini nzuri ya kiislamu ambayo inajali elimu sana. Saudia watu ni vilaza watupu kiasi kwamba kuna Wamisri milioni moja na zaidi wanaofanya kazi za kisomi. Kote huko Ghuba kasoro Yemeni na Omani (kwa sababu ya umaskini wao) kuna wageni wengi ndani ya nchi kuliko wenyeji kwa sababu watu hawataki shule.

10. Waislamu wa pwani ya Tanzania, kama wenzao wote wa Somalia yote, Lamu, Malindi, Mombasa, Zanzibar, Mafia, Kilwa, Lindi na Pemba ya Msumbiji, wana utamaduni wa Waarabu wa Ghuba wa kugomea shule. Tofauti na wenzao, waislamu wa Tanzania walioko Machame na Usangi mkoani Kilimanjaro, au Bukoba, na hata wale wa kabila la Waganda (Baganda) kule Uganda, wao wanapenda shule. Maeneo yote waliyokaa Waarabu, kuanzia Bagamoyo nenda hadi Tabora/Nzega, na Ujiji, shule si mali kitu. TATIZO SI UISLAMU BALI UARABU WA GHUBA. Anayebisha hongera zake.

11. Tafiti mbili ninazozijua, nitazisaka baadaye, zinasema kwamba kwenye miaka ya nyuma kama ya 1990, pale UDSM waislamu walikuwa ni kati ya 14 - 15% ya wanafunzi wa shahada ya kwanza wote. Hiki ni kiasi kidogo mno lakini ni kidogo cha kiasi gani? Lazima tujue hili nalo, hata kwa makadirio tu.

12. Nyerere aliamua tuachane na sensa ya kupekua dini za watu kwa sababu nzuri kabisa - alitaka Watanzania tusitambuane kwa dini zetu (na makabila pia). Hivyo, ili kuweka usawa tukaanzisha msemo huu: Tanzania sisi nusu ni Waislamu na nusu ni Wakristo. Huu ni msemo tu na hauna usahihi. Pili, hata kama sensa ya zamani ilionesha kwamba waislamu ama wakristo au wapagani ndio wengi, haina maana yoyote leo wakati taifa letu lina watu milioni 45 hivi. Tulipata uhuru tukiwa milioni 12 na baadaye Zanzibar ikaongeza laki tatu. Watanzania hatukuwa na kelele za asilimia ngapi ni dini hii na ile. Leo zimerudi.

13. Kwa mujibu wa taarifa za kitafiti (siyo mimi), Waislamu nchini Tanzania ni theluthi moja ya watu wote. Naomba Nasser na Salim muende mkamuulize rais wetu, Jakaya Kikwete, kwamba kwa nini alipoteua mawaziri mwaka Novemba 2010 aliweka theluthi moja waislamu, na kisha manaibu akafanya hivyo hivyo? Pia, muulizeni, kwa nini alipoteua mawaziri hii juzi, aliweka 1/3 waislamu na kwenye manaibu akafanya hivyo hivyo? Kabla hamjaenda, chukueni rekodi zenu kwanza muone. Jiulizeni pia, kwa nini wajumbe wa Tume ya Kupitia Katiba ya Muungano, wale wa Bara, theluthi moja tena ni waislamu? Rais Kikwete, nijuavyo mimi, anajaribu sana kuliangalia hili suala la kelele za dini ili asiharibu nchi yetu. Anakuwa mwangalifu sana, hata kama kuna wakati anateleza. Je, mahesabu yake haya yana maana gani? Nina hakika anajua anachokifanya na kamwe hawezi kuwaonea waislamu wenzake ambao ni Watanzania kama yeye. Hawezi kufanya uonevu.

14. Zifuatazo ni taarifa zinaonesha idadi ya waumini wa kiislamu nchini Tanzania:

(i) 35% = http://www.qran.org/a/a-world.htm.
(ii) 29 - 35% = http://en.wikipedia.org/wiki/List_of_countries_by_Muslim_population or The Future of the Global Muslim Population (Pew Research Center), http://pewforum.org/future-of-the-global muslim-population-preface.aspx
(iii) 35% = http://www.state.gov/j/drl/rls/irf/2010_5/168434.htm.

15. Hiyo taasisi ya kwanza ni ya kiislamu. Sijaweka za Wakristo kwa sababu sitafuti ushindani na siamini kama idadi ina maana yoyote, lakini kwa kuwa watu mnataka kupigia kelele, basi mzigo huo hapo. Mwaka jana mwanaharakati mmoja wa Tanga alikuja Marekani na akasema mkutanoni kwenye chuo kikuu kimoja kwamba waislamu ni 70% ya Watanzania wote, na pia kuna mwislamu mmoja mwenyeji wa Songea aliandika makala ya kitaaluma na akasema kwamba waislamu Tanzania ni 55% lakini akashindwa kueleza wanaishi wapi. Huyu wa 70% alishindwa pia kusema wanakaa wapi ambako hawaonekani. Pointi ni kwamba madai haya ni ya kijinga. Makala nyingine iliyoandikwa na msomi huyu Mtanzania ilisema kwamba Uganda wapo 45% na Kenya 33% na Msumbiji 40% (kama sijakosea). Hakuna popote duniani, hata kwenye mashirika ya kimataifa ya kiislamu zinapotajwa namba hizi za 55% kwa Tanzania na hao wengine wa Afrika Mashariki. Mashirika ya kiislamu yanasema kwamba Tanzania ina 30 - 35% tu. Ili kuleta amani, naomba tuseme kwamba Tanzania haina Wakristo kabisa, hata mmoja hayupo isipokuwa wale wenye madaraka serikalini. Tukumbuke pia, marais wetu wote watano wa sasa (kule Zenji na kwenye Muungano) ni waislamu.

16. Kwa nini idadi inakuwa muhimu hapa, achilia mbali kelele? Ni kwa sababu tunataka kuielewa ile 14-15% ya UDSM ambayo huenda hivi leo imeshabadilika kwa kuwa tuna vyuo vingi nchini. Tunahitaji maelezo, kwamba hao waislamu wengine wameishia wapi? Jibu lake linarudi kwenye ule UTAMADUNI WA WAARABU WA GHUBA. Hakuna mwislamu anayeonewa wala anayenyimwa shule. Mimi nimekulia na kusomea Dar es Salaam kwenye waislamu wa kutosha kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, na JKT kabisa. Waislamu wote marafiki zangu waliokuwa wakali darasani waliendelea na elimu ya juu. Shule ya msingi tulikuwa watoto wanne machachari, mimi, Waziri, Salum na Izihaki, na wote tulifaulu. Vijana wa mwaka mmoja nyuma yetu pale Azania walikuwa na Mpemba aliyepata pointi SABA. Alikwenda tena Tambaza akawa nyuma yetu na akapata pointi TATU. Akaenda Ulaya. Hakunyimwa nafasi yoyote. Mwaka niliomaliza kidati cha sita kijana aliyeongoza Tanzania nzima alikuwa Karim, na yeye pia mwislamu. Hao wanaonyimwa wako wapi?

17. Kwa hiyo, kama 1/3 tu ndio waislamu (walau kinadharia), na pia wengi wao wako pwani kwenye utamaduni wa Ghuba usiotaka shule, tunashangaa nini wakienda wachache vyuo vikuu, tuseme 20%? Je, watakuwaje sawa serikalini na Wakristo ambao walianza utamaduni wa elimu tangu enzi hizo? Ni suala la historia tu lakini si kwamba ukiwa mwislamu huwezi kwenda shule.

OMBI

Tufanye juhudi kuwakomboa wale wote walio nyuma kielimu Tanzania. Wako wengi, kwa dini na makabila, lakini wote ni Watanzania. Walio nyuma wasiseme kuna uonevu, bali waondoe kilichowakwamisha. Hatuwezi kulinganisha utamaduni wa elimu wa watu wa Kilwa, Mafia, Rufiji na Pangani, na watu wa Moshi, Kyela, au mkoani Kagera. Tuwe wakweli. Mwenyezi Mungu hapendi waongo. Kwa nini shule za binafsi hazina pia waislamu wengi? Nani anawazuia waislamu kujenga shule Tanzania? Je, kama kweli unataka mtoto wako apate elimu safi, na amekosa nafasi ya shule ya serikali, utampeleka wapi? Pale Kinondoni Muslim? Tuseme ukweli.

Naamini tunao uwezo wa kuyatatua matatizo yetu ya kihistoria na kitamaduni na si kukaa chini kupanga vurugu kwa madai ya kuonewa. Waislamu wa Saudi Arabia hawajasoma licha ya utajiri wao. Je, hao nao waziri wao wa elimu na baraza la mitihani ni ya Tanzania? Kwani waislamu wa Uturuki, Tunisia, Misri, Senegal na Afrika Magharibi yote wana elimu?

Tutafute chanzo cha kweli cha tatizo, halafu wote tushirikiane kulitatua; wote kabisa.

AOTA MATITI BAADA YA KUTUMIA ARV's


Mkaazi wa kijiji cha Magomeni Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani,  Khamisi Tanga (46), ameota  matiti katika hali isiyo ya kawaida ikidaiwa imesababishwa na kutumia dawa za kupunguza  makali ya Ukimwi   ARV’S.  

 Akizungumza na waandishi wa habari waliokwenda Wilayani humo kufanya utafiti kuhusu utekelezaji wa sheria ya Ukimwi na Chama cha Waandishi wa habari za Ukimwi (AJAT),Khamisi (Pichani) alisema alipatwa na mkasa huo miaka mitatu iliyopita.    Akisimulia namna alivyoanza kuugua alisema awali aliona matiti yake yakiongezeka ukubwa kila kukicha lakini hakujua kama lingeweza kuja kuwa tatizo kubwa kama lilivyo sasa.    Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ilimbidi kwenda kliniki anayohudhuriaga kupata dawa na kuwaeleza manesi ambapo walimjibu kuwa imesababishwa na dawa anazotumia na hivyo kulazimika kukatizwa dozi hiyo na kupewa aina nyingine.
   
Hata hivyo Khamisi alisema kwamba pamoja na kubadilishiwa dozi hajaona kama kuna mabadiliko yoyote aliyoyapata na kuongeza kwamba hivi karibuni alipewa dawa nyingine ambazo kati ya hizo kuna zile ambazo zilimsabishia matiti na tayari ameanza kupatwa na maumivu aliyokuwa akisikiaga awali wakati matiti yalivyokuwa yanaanza kuota.

Kwa mujibu wa Khamisi ameshahangaika kupata matibabu hadi Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili lakini hadi leo hajapatiwa tiba stahili ya kumaliza tatizo hilo.    “Jamani Watanzania naomba wanisaidie kwa njia yoyote ile ili niondekane na hali hii kwani inanidhoofisha sana na kunikosesha raha hasa mbele ya wanaume wenzangu."Kwani hapa navyoongea na nyie waandishi nilipimwa hadi kansa na matiti ndio kama hivyo mnavyoyaona yanaendelea kukua na huniuma sana hasa wakati ninapolala,”alisema Khamisi  

Pia ametumia fursa hiyo kumuomba Rais Jakaya Kikwete kumsaidia ili arudi katika hali yake ya uanaume kwa kuwa maisha kwa sasa kwake yamezidi kuwa magumu kwa kuwa hawezi kufanya kazi yoyote kutokana na hali hiyo.

Mtaalam wa magonjwa, Dk. Dina Komakoma,akielezea kuhusu sababu za kutokewa kwa hali hiyo kwa wagonjwa wenye maambukizi ya VVU ni jambo la kawaida japo hutofautiana.Dk. Komakoma alisema wengine hujikuta wakinenepa au wakikonda sana na hili la Khamis sio mtu wa kwanza kupatwa na hali hiyo na kuongeza kwamba inapotokea mgonjwa akapata hali tofauti kama hiyo anapaswa kusitishiwa dawa.

 kwa hisani ya MICHUZI