Mkaazi wa kijiji cha Magomeni Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani,
Khamisi Tanga (46), ameota matiti katika hali isiyo ya kawaida
ikidaiwa imesababishwa na kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi
ARV’S.
Akizungumza na waandishi wa habari waliokwenda Wilayani humo kufanya
utafiti kuhusu utekelezaji wa sheria ya Ukimwi na Chama cha Waandishi wa habari
za Ukimwi (AJAT),Khamisi (Pichani) alisema alipatwa na mkasa huo miaka mitatu
iliyopita. Akisimulia namna alivyoanza kuugua alisema awali aliona
matiti yake yakiongezeka ukubwa kila kukicha lakini hakujua kama lingeweza kuja
kuwa tatizo kubwa kama lilivyo sasa. Baada ya kuona hali inazidi
kuwa mbaya ilimbidi kwenda kliniki anayohudhuriaga kupata dawa na kuwaeleza
manesi ambapo walimjibu kuwa imesababishwa na dawa anazotumia na hivyo
kulazimika kukatizwa dozi hiyo na kupewa aina nyingine.
Hata hivyo Khamisi alisema kwamba pamoja na kubadilishiwa dozi hajaona
kama kuna mabadiliko yoyote aliyoyapata na kuongeza kwamba hivi karibuni
alipewa dawa nyingine ambazo kati ya hizo kuna zile ambazo zilimsabishia matiti
na tayari ameanza kupatwa na maumivu aliyokuwa akisikiaga awali wakati matiti
yalivyokuwa yanaanza kuota.
Kwa mujibu wa Khamisi ameshahangaika kupata matibabu
hadi Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili lakini hadi leo hajapatiwa tiba stahili ya
kumaliza tatizo hilo. “Jamani Watanzania naomba wanisaidie kwa
njia yoyote ile ili niondekane na hali hii kwani inanidhoofisha sana na
kunikosesha raha hasa mbele ya wanaume wenzangu."Kwani hapa navyoongea na
nyie waandishi nilipimwa hadi kansa na matiti ndio kama hivyo mnavyoyaona
yanaendelea kukua na huniuma sana hasa wakati ninapolala,”alisema Khamisi
Pia ametumia fursa hiyo kumuomba Rais Jakaya Kikwete kumsaidia ili arudi
katika hali yake ya uanaume kwa kuwa maisha kwa sasa kwake yamezidi kuwa magumu
kwa kuwa hawezi kufanya kazi yoyote kutokana na hali hiyo.
Mtaalam wa magonjwa, Dk. Dina Komakoma,akielezea
kuhusu sababu za kutokewa kwa hali hiyo kwa wagonjwa wenye maambukizi ya VVU ni
jambo la kawaida japo hutofautiana.Dk. Komakoma alisema wengine hujikuta
wakinenepa au wakikonda sana na hili la Khamis sio mtu wa kwanza kupatwa na
hali hiyo na kuongeza kwamba inapotokea mgonjwa akapata hali tofauti kama hiyo
anapaswa kusitishiwa dawa.
kwa hisani ya MICHUZI
No comments:
Post a Comment