Shujaa wa Kilimo aliyekatwa Mikono akidai Mahari



PAMOJA na kuwa na ulemavu wa kutokuwa na mikono yote miwili, Salim Mbela mkazi wa eneo la Delux, nje kidogo ya mji wa Songea, amefanikiwa kulima shamba la mahindi kubwa na zuri kwa kutumia miguu yake.

Ukiliona shamba hilo la Mbela licha ya kuwa na mahindi, pia lina maharage, magimbi na ndizi yaliyostawi na kupendeza.
Huwezi kuamini kuwa shamba hilo linalimwa na Mbela, ambaye ni mlemavu kwa kutumia miguu yake.

Ulemavu huo umemkuta na kulazimika kulima kwa miguu, baada ya kukatwa mikono yake alipokuwa akidai kurejeshewa mahari kutoka kwa wakwe zake.
Mbela anasema kuwa pamoja na ulemavu alioupata ukubwani, hawezi kutembea mitaani kuomba omba, wakati bado mwili wake una viungo vingine anavyoweza kuvitumia kujipatia mahitaji yake ya kila siku.

Kilichosabisha kukatwa mikono

Mbela alizaliwa miaka 53 iliyopita akiwa na mikono miwili na mwenye afya tele, lakini misukosuko ya maisha imemfanya leo abaki hana mikono yake miwili, huku akiishi peke yake.
Anaeleza kuwa kabla ya kuwa mlemavu, aliwahi kuajiriwa na Jeshi la Polisi, akifanyia kazi Kituo cha Polisi Makuyuni mkoani Arusha miaka ya nyuma, lakini alicha kazi hiyo baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Baada ya hali hiyo, aliona bora arudi nyumbani kwao Kijiji cha Malumba wilayani Tunduru ili kuendelea kupata matibabu.
Mbela anasema kuwa alipofika kijijini kwao, aliendelea kupata matibabu na baadaye akapona.

Akizungumza kwa kusaidiwa na rafiki yake wa karibu ambaye amejitambulisha kwa jina la Zacharia Dikala, maarufu kama Babu Masai, Mbela anasema kuwa alikutana na matatizo ya kukatwa mikono miaka minne iliyopita.
Mbela ambaye pia ni baba wa watoto Mwanabibi Salim (28), Siku Salim (19) na Said Salim (24) anaeleza kuwa akiwa na mkewe na familia yake, siku moja ali kwenda nyumbani kwa wakwe zake waliokuwa wakiishi katika kijiji hicho cha Malumba na kuchukua mbuzi wake aliotoa mahari miaka ya nyuma wakati akimchumbia mkewe ambaye ndiye aliyemzalia watoto hao.
Anasema kuwa wakati huo alikuwa na nguvu na alitumia mabavu kufanya fujo, hadi akafanikiwa kufika zizini na kupora mbuzi, bila kujua kama maisha yake yange badilika na kuishia pabaya.

Hata hivyo, anajutia kitendo hicho akisema kwamba iwapo angefahamu mapema yataka yomkuta, asingethubutu kwenda kufanya fujo hizo.
“Nilikuwa najiamini sana, nilikuwa na nguvu sana, nikaamua kwenda ukweni kwangu kufuata baadhi ya mifugo yangu, niliyotoa mahari wakati namposa mke wangu,” anasimulia na kuongeza:
“Nilipofika ukweni, niliingia zizini moja kwa moja na kufungua mbuzi kwa lengo la kwenda kuwauza ili nipate fedha, lakini kwa bahati mbaya kwa kuwa ilikuwa ni usiku, walipiga kelele na mimi kwa ubabe wangu nikawafanyia fujo sana wakwe.”
Anafafanua: “Hivyo, waliitwa mgambo kutoka Kata ya Malumba, walipofika nilipambana nao, lakini walinishinda na walifanikiwa kunipiga sana, kisha kunifunga mikono yangu miwili kwa nyuma kutumia mipira, wakanipeleka na kunitupa porini. Ukweli niliteseka sana hadi nilipookotwa nikiwa sijitambui.”

Anasema kuwa baada ya mkasa huo alipoteza fahamu, alipozinduka, alijikuta akiwa amelazwa Hospitali ya Mbesa, wilayani Tunduru huku mikono yake ikiwa imeharibika vibaya na hakukuwa na njia nyingine, zaidi ya kukatwa mikono yake yote miwili na kulazwa hospitalini hapo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Naumia, nimepoteza mikono yangu kwa uzembe. Ningejua kama yangenikuta haya, nisingefanya fujo zile, ila nashukuru Mungu nipo salama na maisha yangu yanaendelea,” anasema Mbela.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo za maisha, Mbela hajakata tamaa, bali anaendelea na maisha yake kama walivyo watu wengine katika eneo analoishi.
Zacharia ambaye ni rafiki mkubwa wa Mbela anasema kuwa tangu apoteze mikono yake, Mbela hakupenda tena kuendelea kuishi katika kijiji hicho, bali alilazimika kuondoka na hadi Songea mjini ambapo alifikia kwa ndugu zake eneo la Luhila na kukaa nao kwa muda, hadi walipomfukuza kutokana na tabia yake ya kubeba mizigo kwa kutumia midomo waliyodai inawakera .
“Kwa sasa anaishi peke yake katika nyumba chakavu ya Shirika la Umeme  Tanzania, (Tanesco), iliyopo Songea, huku akijilimia shamba lake kwa kutumia mguu, ambapo hatumii jembe, badala yake hutifua ardhi na kupanda mazao mbalimbali kwa kutumia mdomo. Pia anapalilia mazao yake yakiwamo maharage, mahindi, magimbi pamoja na ndizi kwa kutumia mdomo,” anaeleza Zacharia.
“Maisha yangu yamebadilika sana , nimetengana na familia yangu, ingawa huwa wanakuja kuniona mara moja moja, hata mke wangu, lakini najihisi upweke sana,” anasema akifafanua:
“Nafanya kazi zangu mwenyewe na nalima mazao mbalimbali ya chakula, napata chakula changu na kingine nahifadhi kwa ajili ya familia yangu. Napata gunia tatu badala ya nane kutokana na watu kuniibia mahindi yangu yakiwa mabichi hata yakikauka. Inaniumiza, ila sina jinsi.”

Mbela anataja changamoto mbalimbali anazokutana nazo kuwa ni kuibiwa mazao yake na baadhi ya vijana aliodai ni majirani zake wasio waaminifu, hali ambayo imemsababishia kukorofisha nao na yeye kuwekwa ndani zaidi ya mara mbili .
Anasema, amekuwa akipambana na wezi wake kutumia miguu kwa kuwapiga na kuwakanyaga na akitoa onyo kwa watu wenye tabia ya kumwibia mazao yake kuacha vitendo hivyo.
Polisi huyo mstaafu ameiomba Serikali kumsaidia kwa kumpatia mbolea ya ruzuku walau mfuko mmoja, ili aweze kuzalisha mazao kwa wingi zaidi, pamoja na watu walio na mapenzi mema ku msaidia ili aweze kuendesha maisha yake na familia yake.