Kinabo mhitimu SUA aliejiajiri katika ufugaji wa samaki

Mawazo ya wahitimu wengi wa vyuo vikuu nchini katika miaka ya karibuni  imekuwa ni namna ya kupata  ajira zenye tija. 
Ndoto ya wengi ni kupata kazi za kipato kizuri na ambazo zitawawezesha kuishi vizuri, kumiliki gari, kujenga nyumba na mambo mengine lukuki.
Hata hivyo, baadhi wamekumbana na tatizo la ajira ambalo limewasukuma katika kubuni miradi ambayo  itawawezesha kumudu maisha na changamoto zake.

Mmoja wao, Simon Kinabo, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichoko Morogoro ameamua kujiajiri baada ya  kubuni mradi wa  ufugaji wa samaki.
Mradi huo  unaoitwa Rombo Unique Aquaculture, upo kilomita 60 kutoka mjini Moshi na kilomita nne kutoka makao makuu ya Wilaya ya Rombo, eneo la Mkuu.
Anasema akiwa mwanafunzi katika chuo hicho, akisomea Shahada ya Sayansi ya Viumbe wa Majini (BSc Aquaculture) alihamasika na somo la uzalishaji wa samaki na ndipo akaamua kuanzisha mradi huo kwa mtaji wake.
“Katika fedha zile za mkopo,  kila nikipewa na Serikali, nilichukua kiasi kidogo na kuanzisha nyumbani mradi wa kufuga samaki.
Niliamini ni mradi mzuri ambao unaweza kubadili maisha yangu,” anasema.
Anaongeza kuwa alianzisha mradi huo  kwa kuchimba bwawa dogo na kuanza kuzalisha samaki, kwa lengo la kuja kuwauza baadaye.

Mkopo wa CRDB
Anasema akiwa mwaka wa pili SUA  alipata taarifa ya kuwapo mradi wa SUGECO unaoendeshwa na chuo hicho na CRDB ambao unalenga kuwawezesha wanafunzi wa elimu ya juu kuingia katika ujasiriamali.
“Baada ya kupata taarifa hizo nilijitokeza kuandika andiko la kuomba fedha na baada ya usaili, andiko langu lilipitishwa na chuo na CRDB,” anasema.
Anaongeza kuwa baada ya kupitishwa andiko lake, alipokea mkopo wa Sh20 milioni kwa ajili ya kuanzisha mradi.
Baada ya kupokea fedha, aliamua kupanua bwawa  hilo na pia kuliongezea mifumo ya kuingiza maji kutoka Mto Ngwasi na kutoamaji ili liwe la kisasa.
“Nilinunua mabomba 100 ya futi 2,000 na sasa bwawa langu lina urefu chini, mita  tatu hadi sita na upana mita 30,” anaeleza.
Anasema kuwa baada ya upanuzi wa bwawa alinunua samaki wadogo 3,000 kutoka Gereza la Karanga mjini Moshi ambao walikuwa ni  wa jamii ya perege na kambare.
Anaongeza kuwa  kila kifaranga cha samaki alikinunua kwa Sh300 na kwamba hiyo ilikuwa Mei 5, mwaka  jana, alipoanza kuwapandikiza bwawani mwake.

Mafanikio ya mradi
Hadi sasa, Kinabo anasema bwawa lake linao  zaidi ya samaki  40,000, kati ya hao wakubwa ni 10,000 na wadogo 30,000.
Anasema , Juni mwaka huu  anatarajia kuanza kuvua samaki na  matarajio yake  ni kuvua tani  nne  za samaki.
“Nina imani tani hizo nne, nikivua naweza kupata zaidi ya Sh60 milioni na tayari nimepata masoko,” anasema  msomi huyo.
Anasema tayari, amefanya mazungumzo na wakuu wa shule kadhaa za sekondari  wilayani Rombo, Hospitali ya wilaya hiyo na maeneo kadhaa ambao wamekubali kununua samaki wake.
Kwa kutambua kuwa hawezi kufanya kazi  hizo peke yake, mjasiriamali huyo msomi amemwajiri mtunza mazingira, James Edmund,  pia hivi karibuni atakuwa na walinzi wawili na muuzaji wa samaki.

kwa hisani yamwanachi