Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwishoni mwa wiki limepitisha kwa kauli moja Tamko la Kisiasa kuhusu Utatuzi wa Migogoro Barani Afrika kwa njia ya Amani.
Tamko hilo ambalo ndani yake
linaainsha na kutambua mchango mkubwa wa Muungano wa Nchi
Huru za Afrika (OAU) na sasa Muungano wa Afrika ( AU) katika
kuchagiza na kusimamia pamoja na mambo mengine, maendeleo ya nchi
za Afrika na watu wake, kupiga vita umaskini, ujenzi wa utawala
bora, demokrasia , haki za binadamu na utatuzi wa migororo kwa njia za
amani.
Kabla ya kupitishwa kwa Tamko hilo,
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa siku nzima ya Alhamisi na
ijumaa asubuhi lilijikita katika majadiliano ya mada iliyohusu
‘utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani barani afrika’, ikiwa pia ni sehemu
na Baraza hilo kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa
kwa OAU na baadaye AU.
Miongozi wa viongozi wakuu walioshirikia
majadilaino hayo, na ambayo yaliandaliwa na Bw. Vuk Jeremic, Rais
wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki
Moon, Rais wa Equatoria Guinea Theodore Obiang Nguema
Mbasogo, Rais Mstaafu wa Burundi Jean Pierre Buyoya ambaye
pia Mwakilishi maalum wa Muungano wa Afrika
huko Mali na Sahel, wakiwamo pia mawaziri kadhaa wa Mambo ya
Nchi za Nje.
Akiungana na wazungumzaji wengine katika
mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako
Manongi, pamoja na kuainisha sababu na vyanzo vya migogoro Barani Afrika,
alisema, Afrika lazima ifikie mahali ikatae kugawanywa.
“Bara la Afrika lina fursa
nyingi, Afrika inapanda chati. Afrika lazima ikatae kugawanywa, ikatae
kudharauliwa na ikatae kunyonywa” akasema Mwakilishi wa Kudumu, Tuvako
Manongi.
Na kubainisha kwamba, Afrika lazima
pia ikatae kutambuliwa kama bara ambalo limejaa migogoro . “ Huu ni
wakati wa kufufua upya pan africanism, hiki ni kipindi
cha mwamko mpya wa Afrika. Lazima tufanye kazi kwa pamoja ili kuwapa
matumaini watu wetu” akasisitiza Manongi.
Wakati tukisherehekea maadhimisho ya
miaka 50 wa OAU, ni vema kila mmoja wetu akaahidi upya
kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na
Muungano wa Afrika kama
ilivyoainishwa katika Sura ya Saba ya Katima ya Umoja wa
Mataifa.
Akatoa mfano kwa kusema uhusiano
huo unapashwa kuendelezwa katika nyanja zote za usalama na
maendeleo. Kama ambavyo imeshashuhudiwa katika
uundwaji wa Jeshi la Mseto kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa
Afrika katika Jimbo la Darfur ( UNAMID), Misheni ya
Muungano wa Afrika huko Somalia, (AMISOM0 na tukio la hivi karibuni la
kurejewa na kuongozewa uwezo mpya Misheni ya Kutuliza Amani katika DRC (
MONUSCO) kulikoendana na kuridhiwa upelekaji wa Brigedi Maalum inayoundwa
na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi.
Aidha akasema majadiliano hayo ya
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, yamefanyika ikiwa ni siku chache
tu, tangu kufanyika kwa Mkutano wa Baraza la Usalama la Afrika
katika ngazi ya Mawaziri nchini Tanzania, mkutano ambao pia ulijadili kwa
kina pamoja na mambo mengine hali ya usalama barani afrika , vyanzo
vya migogoro na ufumbuzi wake.
Karibu wazungumzaji wote wakiwamo wawakilishi
wa Marekani na Jumuiya ya Ulaya waliochangia majadialiano hayo ya utanzuaji wa
migogoro kwa njia ya amani, licha ya kutambua, kusifu na kupongeza kazi
kubwa ambayo imefanywa na inaendelea kufanywa na Muungano wa
Afrika na Taasisi za Kikanda katika kipindi cha miaka 50 iliyopita,
walisisitiza haja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendeleza
ushirikiano wake na Muungano wa Afrika.
Aidha wazungumzaji huo walitambua na
kukiri kwamba Bara la Afrika licha ya changamoto mbalimbali
zikiwamo za migogoro inayoibuka hapa na pale, imepiga hatua kuubwa za
kimaendeleo, kiuchumi na kijamii na kwamba Bara hilo linastahili
kupongezwa na kuendelea kusaidiwa.
No comments:
Post a Comment