UTAFITI wa kihabari uliofanywa
na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Machi 2012
umefanikisha kumrudisha shuleni mwanafunzi wa sekondari aliyekuwa ametelekezwa
yeye pamoja na familia yao.
Mwenjuma Magalu ambaye kwa sasa
ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Komnyang'anyo
alitelekezwa na babayake yeye pamoja na mamayake mwaka jana, hivyo kushindwa
kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo licha ya kuchanguliwa kuendelea
na masomo.
Hata hivyo baada ya utafiti wa
kihabari kufanyika kijijini Msasa Wilaya ya Handeni na taarifa za mtoto huyo
kushindwa kujiunga na sekondari baada ya mamayake (kwa sasa marehemu) kukosa
uwezo kuripotiwa, alijitokeza mfadhili wa kumsomesha ambaye anagharamia masomo
yake hadi sasa.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi juzi akiwa shuleni Komnyang'anyo, mwanafunzi huyo aliishukuru TAMWA
kwa kuibua tatizo la familia yao kwa umma na kupatikana kwa mfadhili ambaye
amemrudisha masomoni licha ya familia yao kutelekezwa.
"Binafsi nawashukuru sana
hao (TAMWA) waliopaza sauti hadi mjuu wangu kurudi shuleni...hii kwetu ilikuwa
ni ndoto kwetu maana mtoto mwenyewe alikuwa amekata tamaa kabisa kurudi shuleni
na alikuwa kaanza kufanya vibarua mitaani huku wenzake wakiendelea na
shule," alisema bibi wa mtoto huyo, Amina Mohamed akizungumza.
Bibi huyo akizungumzia maisha
ya sasa ya familia hiyo alisema bado wanahitaji msaada wa huduma hasa baada ya
mwanaye kufariki dunia mwaka jana na kumuachia watoto wake.
Aliongeza kwa sasa yeye ni
mgonjwa wa TB anayetumia dawa hivyo kwa hali yake ameshauriwa kupumzika jambo
ambalo limempa mzigo mkubwa kimajukumu mwanafunzi (Mwenjuma), kufanya kazi za
nymbani kama kupika kulima na shughuli nyingine.
Hata hivyo mama wa mtoto huyo
(Hadija Magalu) ambaye alitelekezwa na mzazi mwenzake alifariki dunia mwaka
jana kwa tatizo la uzazi na kuiacha tena familia hiyo ya watoto watatu katika
hali ngumu zaidi chini ya malezi ya bibi mzaa mama.
kwa hisani ya mjengwablog
No comments:
Post a Comment