KATIKA HILI WATANZANIA TUMEMSAHAU GADDAFI!!

  Inaelekea waTanzania wengi wamesahau historia kati ya Libya na Tanzania. Marehemu Gaddafi alikuwa rafiki yake mpenzi nduli mshenzi Dikteta Idi Amin Dada wa Uganda!  Gaddafi alitaka Amin amwoe binti yake! Gaddafi alituma wanajeshi kutoka Libya kuwasaidia Uganda katika vita vya Kagera mwaka 1978-79.  Sisi wazee tunaikumbuka hio vita na miezi kumi na nane (miaka 18) ya shida iliyofuata!  Maoni chini yameandikwa na mwanachama la kundi - Wanabidii

Kanali Gaddafi alipotembelea Uganda mwaka 1978

...Wanabidii!


  
Binafsi nachukia sana kuandika bila ya ushahidi! Na zaidi sipendi kuandika "propaganda" na taarifa za uzushi; isipokuwa napenda kuandika taarifa zilizotafitiwa kwa kuandikwa na mtafiti mwenyewe (na au mwandishi aliyeandika matokeo ya utafiti au kufanya upembuzi wa utafiti husika). Takriban wiki moja sasa (tangu Alkhamis ya tarehe 20 Oktoba, 2011) uwanja wa "Wanabidii" na majukwaa mengine ya kijamii yamekuwa yakijadili "Kuuawa kwa Kanali Muammar Gaddafi" kulikofanywa na wale wanaoitwa waasi (wa NTC) wakisaidiwa na NATO wakiongozwa na Uingereza, Marekani, Ufaranza na washirika pamoja na Waarabu (Saudia na Qatar). Gaddafi ameuawa; kwa jinsi gani, kila mmoja amesoma, ameona (kwenye picha za mndato) na au kwenye picha za video!

  
Ninachotaka kuandika na pengine kuanzisha "mjadala" wa kiakili ni juu ya "GADDAFI KUMSAIDIA IDI AMIN DADA KWENYE VITA VYA KAGERA [UGANDA DHIDI YA TANZANIA MWAKA 1978 HADI 1979]". Napenda niweke wazi kwamba, "historia haisomwi ili kufufua 'chuki' bali husomwa kujua yaliyopita, kuyasanifu yaliyopo na kupanga mipango kwa yajayo!". Hivi ndivyo tunavyosoma historia iwe yenye kuhuzunisha au kufurahisha! Tanzania ilipigana vita na Uganda, vita iliyoitwa VITA YA KAGERA (japokuwa ilipiganwa hata ndani ya Uganda na Idi Amini Dada kufurushwa na kuikimbia Uganda!).

Kwa ujumla, tangu pale kifo cha Muammar Gaddafi kilipotangazwa kwa mara ya kwanza na kituo cha runinga cha Al-Jazeera na kukaririwa na vituo vingine na mashirika ya habari ya kimataifa kama BBC, CNN, Reuters, Xinhua, AFP, AP na IRNA (Press Tv) kumekuwa na mkanganyiko wa "mawazo" kwa wananchi wa Tanzania juu ya "hali" ya Gaddafi kisiasa katika mtazamo wa kifalsafa...hususan wengi wa wachangiaji kwenye mijadala hiyo wanamuona Muammar Gaddafi kama "shujaa" na "mwanamapinduzi" na "kiongozi mtukuka" na "aliyejitolea kuunganisha Afrika" na hata wengine kufikia kiasi cha kuonyesha kwamba hajawahi kutokea kama Muammar Gaddafi na hata kumpa "daraja" ya kuwa "Baba wa Afrika" na mshumaa uliyozimika! Hata hivyo wengi wamesahau kwamba ni Muammar Gaddafi ndiye aliyemsaidia Idi Amin Dada kwenye Vita vya Kagera! Naomba sasa tuangalie nini alifanya Gaddafi wakati wa vita vile.

Vita vinahitaji rasilimali watu (askari na wataalamu wa kijeshi), fedha za kuendeshea vita na zana (za kivita na za mawasiliano ya kivita). Kwa mujibu wa taarifa rasmi na zinazothibitishwa na taarifa rasmi za kihistoria Muammar Gadafi alimpa Idi Amin Dada usaidizi ufuatao:


1. WANAJESHI (WAPIGANAJI) 3,000 (Elfu tatu kutoka Libya na nchi zilizokuwa na mahusiano na Libya ambazo Gaddafi likuwa anazisaida na zenye uzowefu wa mazingira ya vita [military knowhow and skills on interlocustrine terrain]);

2. ZANA KAMA VIFARU AINA YA T-54, T-55, BTR, APCs, BM-21, Katyusha MRLs;

3. MIZINGA na

4. NDEGE ZA KIJESHI AINA YA MiG-21s na Tu-22 Bomber.

  
Wanajeshi wa Libya waliyotumwa Uganda walikuwa katika makundi yafuatayo: ASKARI WA KAWAIDA; WANAMGAMBO; NA ASKARI WA VITA VYA MSITUNI (WENYE UZOEFU WA VITA VYA KIENYEKI KUTOKA JANGWA LA SAHARA [MAARUFU KAMA WATUAREG KUTOKA TCHAD, NIGER, ALGERIA na DARFUR]). Hata hivyo, shukrani za pekee kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) waliofanya kazi ya ziada ya kujitoa mhanga kupigana "kiume" na hatimaye kuyashinda majeshi ya Idi Amin Dada akisaidiwa na Muammar Gaddafi. Hata ilipofika mwezi wa Aprili, 1979 na Idi Amin Dada alipopoteza udhibiti wa nchi ya Uganda aliamua "kuikimbia" Uganda na kituo chake cha kwanza kilikuwa Libya (kwa Muamar Gaddafi) na alipewa "hifadhi" ya muda na baadaye kwenda "uhamishoni" nchini Saudi Arabia (alikoishi hadi kufa kwake akiwa Jeddah).

 
Kwa wasomaji na "wanabidii" na wengine wanaomtazama Muammar Gaddafi kwa kusahau "aliyoyafanya" dhidi ya kumsaidia Idi Amin Dada kuendesha vita na Tanzania nadhani wana wajibu wa kujiuliza masuala haya (hii ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inawajibu wa kusema ukweli):

1. Wamesahau "hadithi" hii ya Vita vya Kagera? Au, vita hivi vilikuwa "propaganda" ya kisiasa?

2. Gaddafi alidhamiria nini kumsaidia Idi Amin Dada aliyeapa kuisambaratisha nchi (Tanzania) na kwa kuanzia aliteka Kagera na kuifanya sehemu ya Uganda?

3. Kama Idi Amin Dada wa Uganda alitangazwa "dikteta", "bundi", "joka", "fisi mla watu", na masimulizi mengine ya kutisha (hata ya kula nyama za watu); mtu aliyekuwa akimsaidia mtu wa aina hiyo (kama Gaddafi) anaitwaje?

4. Je, historia ya Vita vya Kagera iliandikwa kwa wino "gani" hadi leo imesahaulika?

5. Au, wote wanaodhani kwamba Muammar Gaddafi ni "shujaa" wa Afrika wamezaliwa miaka ya 1980? Na kwa jinsi hiyo hawajui kilichotokea kati ya miaka ya 1978 na 1979?

 
Mwisho, siandiki haya katika kuwakumbusha "majonzi" wananchi wa Kagera waliouawa kikatili na Idi Amin Dada; siwakumbushi machungu ya kutiwa vilema vya maisha; siwakumbushi madhila ya "kubakwa" wanawake kulikofanywa na askari wa Idi Amin Dada; na wala siwakumbushi jinsi mali zao (mashamba na nyumba) zilizvyoharibiwa na "ushenzi" wa Idi Amin Dada! Nataka niwakumbushe kwamba, "hatuwezi kurudisha nyuma historia; lakini ni wajibu kuisoma ili vizazi vijavyo vipate kumbukizi yenye kujenga mujtamaa wao." Gaddafi alikuwa "rafiki" na wakati huohuo alikuwa "adui" kwa vile alikuwa na "sura mbili ndani ya moja".

  
Na kwa serikali (iliyoonekana kumuunga mkono); hii ni dhana (binafsi) inawezekana Muammar Gaddafi alilipa sehemu ya "maumivu" ya vita alivyomsaidia rafiki yake mpenzi Idi Amin Dada...kama ndivyo, basi ni vyema watuambie! Hatuwezi kusomeshwa historia ya "uongo" juu ya Muammar Gaddafi kumbe "mtu" huyu (yaani Gaddafi) alikuwa "mtu mwema" na kiongozi "mzuri" kuliko hata Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere...naomba tuwe "wakweli" na kwa kusisitiza: UKWELI UTATUWEKA HURU; KAMA GADDAFI ALIKUWA RAFIKI WA AFRIKA KWA NINI ALIMSAIDIA IDI AMIN DADA KUTUPIGA? TAFAKARI SEMA UKWELI JAPOKUWA UKWELI WENYEWE NI DHIDI YA NAFSI YAKO!
  from.swahiliTimes

1 comment:

Anonymous said...

Labda nianze hivi " We loved him, after sometimes we hate him. Then he became good, thus we had no option we loved him again. Unfortunately, he became even more worse than ever, his rectifications and philosophies made us love him more, at last we were fade up....".

Watanzania sio kuwa wamesahau ila wanaangalia ukweli wa mambo ulivyo. Adui yako ndie huwa rafiki yako. Na lazima ukumbuke jinsi Tanzania (Watanzania)walivoshiriki katika vuguvugu lote la ukombozi wa nchi za Africa toka kwa mikono ya ama mabepari, mabwenyenye na makabaila wa magharibi.

Mi nafikiri watanzania wangekubaliana na kifo cha Gaddafi na pengine wangeshiriki katika yaliotokea Libya kama mtawala wao angekuwa akiwauwa wananchi wake na si waasi katika serikali yake.

Yaliyotokea Libya si yakumfarahisha Mtanzania hata kidogo kwa sababu yale hayakuwa mapinduzi bali ni uasi.

Kinachowatia hofu watanzania ni pale tu nchi za magharibi zitakapotaka kila kilichochetu, nikiwa na maana "Chetu waafrika", kwa mwamvuli wa democrasia ambayo hata kwao haizingaitiwi. Tukumbuke maana ya kitu ni watu wenyewe si maneno "The meaning of something is people and not words" basi kama ndivyo neono democrasia si lazima ifanane na ile ya wamangharibi....!

Ukisema watanzania tumchukie Gaddafi ambaye ni mwizi kwa manufaa ya waafrica kwa sababu tu alimsaidia Idd A. Dada tutakuwa mambumbu tusioweza kujenga falsafa zetu tukingoja kujengewa.

Hata huyo Baba wa taifa JK Nyerere, asingekubalikuona uvamizi wa mataifa ya nje kwa mara nyingine kwa Afrika alliopigania kwa kutumia rasilimali aina zote ( Watu na Mali pengine na Ushauri). Hivyo usiwaone watanzania wakilaani hili ukadhani wamesahau.

Rudisha kumbukumbu zako kwa Namibia walivyosunbuliwa na Muasi Savimbi NATO walikuwapo walichokuwa wakifanya ni kilichoitwa "watching the huma right" ok na Visiwa va Cape Verde Je? Yote hayo maslahi na matumizi ya nafasi yaliyokosekana kwa muda mrefu yaliyopatwa na hiyo tunayoiita NATO.

Ulishawahi kujiuliza kwanini NATO haikuhusisha mataifa yote?

Kwanini iwe kwa Libya tu na si Namibia, Cape Verde, Tunisia na Misri?

Jaribu kupembua zaidi hapo utaona kwannini watanzania hawakupenda namna Gaddafi alivouawa.