Tukumbuke ndugu zangu,mawazo ndiyo mwanzo wa mafanikio yako. Unapokuwa na ndoto mafanikio kwanza yakupasa kuwa na wazo ambalo baadae utalifanyia kazi, ili utengeneze bahati yako. Kwa kufuata maelekezo hayo utakuza upeo wa fikra zako.
Wengi wanaweza wasikutendee haki, kama wengi wafanyavyo, wanaweza kukupotosha katika uhuru ulionao, lakini hawawezi kukuchukulia mawazo unayoyawaza. Kutokana na fikra zako utakuwa unashinda siku zote.
Unataka kuwa na furaha? Unataka kuwa na amani? Unataka kuwa na cheo, nguvu au utajiri? Fikiri kuwa navyo, utafanikiwa. Fikra unazowaza ni muhimu kuliko ujuzi ulionao.
Ujuzi una mipaka, mawazo yanatawala muda wote, yanaleta maendeleo. Kila mtu binafsi anakuwa na ndoto za mafanikio bila kujitambua. Kwa mfano, wazazi wanapopanga ni jinsi gani watawaendeleza watoto wao, wajasiriamali wanapopanga ni jinsi gani wataendeleza biashara zao hiyo yote ni mifano ya kuwa na ndoto njema ya mafanikio. Watu wachache wamejifunza kutumia mawazo yao kwa faida lakini wengi wetu mawazo tuliyonayo yanapata kutu kutokana na kutoyafanyia kazi. Hakuna sababu ya kuona aibu katika dunia ya ubunifu.
Kuwa na mawazo ya kufanya jambo fulani ni kitu kizuri katika dunia hii tunayoishi. Kila mmoja wetu ana kiwanda chake cha kuwa na mawazo. Lakini ni wapi mawazo hayo yanapotoka? Ni wapi waandishi, wana sayansi na wabunifu wanapopata mawazo makubwa? Kwa nini baadhi ya watu wengine wanakuwa wabunifu zaidi ya wengine? Ni kutokana na kutumia vizuri mawazo yao.
Kila mmoja wetu, kwa wakati mmoja au mwingine, lazima kujifunza chanzo halisi cha mawazo. Utajiri, unaweza kuupata, inategemeana na ulivyoyaweka mawazo yako. Wazo dogo rahisi linaweza likabadilisha kabisa maisha yako uliyonayo. Pia huwezi ukajua ukubwa wa mafanikio yako mpaka utakapojifunza jinsi ya kuchanganya juhudi zako na mawazo yako. Kwa vyovyote unapotaka mafanikio unajitathmini wewe mwenyewe. Mwili uliopumzika una nguvu, vile vile akili. Kama unataka kuwa mbunifu na mpokeaji wa mawazo mapya, inakubidi kupata muda kwa mawazo hayo na kuyafanyia kazi.
Jizoeze kila siku kuwa na muda wa mapumziko, chagua chumba kizuri kilichotulia au kiti kizuri ambacho kitakusaidia kutuliza akili kwa urahisi. Unavyoendelea kujifunza kupumzika, utapata mawazo ambayo yatakufikisha katika malengo na matarajio yako.
Mtunzi anafikiri juu ya uimbaji, mchoraji anafikiri juu ya rangi, mwandishi anafikiri juu ya habari na maneno. Kama utachukua wazo moja na kulitendea kazi litakupa matokeo mazuri. Yafanyie kazi mawazo yanayokujia. Kuwa na utayari katika kunasa mawazo yako. Mawazo mengi mazuri yanapotea kwa sababu hayawekwi katika maandishi.
Tathimini mawazo yako. Mara tu unapomaliza kuyachuja mawazo yako, unachagua yale unayotaka kuyafanyia kazi. Utagundua kuwa nayo yanahitaji kuongezewa ubora wake. Jifunze ndugu yangu kutokufunga milango yako ya kuwa mbunifu.
Makala hii imetoka kwa Seif Kabele