Mkasa mwingine wa Kusikitisha St. John University



Mwanafunzi wa uuguzi katika chuo Kikuu cha St. John kilichopo mkoani Dodoma na ambaye alikuwa muuguzi katika hospitali ya Kilimatinde, Manyoni, Singida amefariki dunia baada ya kubakwa na kisha kuuawa na watu wasiojulikana.

Mwili wa marehemu huyo aliyetambuliwa kwa majina Lyidia Mzima mwenye umri wa miaka 57, ulikutwa umetupwa kichakani na tayari ulishaliwa na fisi.



Inataarifiwa kwua marehemu alipatwa na masaibu hayo alipokuwa ametoka kujisomea, akiwa anarudi anakoishi katika nyumba ya kupanga, Kibaoni-Image B, katika kata ya Kikuyu Kusini, iliyopo karibu na chuo hicho.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amethibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi usiku na kwamba marehemu alionekana kunyofolewa nyama za mapajani.

Kiongozi wa wanafunzi wa chuo hicho aliongeza kuwa aliuona mwili wa marehemu ukiwa umechunika ngozi kuanzia utosini hadi sehemu ya kisogoni.

Mwili wa marehemu uligunduliwa na wananchi ambao walisema kwa siku mbili ilikuwa ikisikika milio ya sauti za fisi kutoka katika eneo ambapo mwili wa marehemu ulikutwa.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Dodoma ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Gabriel Mwaluko alithibitisha tukio hilo na kusema hayo yote yanatokana na chuo kukosa mabweni ya wanafunzi kulala jambo ambalo linafanya wanafunzi wengi kwenda kupanga mitaani na kukumbwa na matukio mbalimbali.

Mei mwaka jana, wanafunzi wa chuo hicho waligoma kuingia madarasani hadi wawasilishe malalamiko yao kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kupigwa nondo, kuibiwa vitu kulawitiwa na hata kubakwa. Walisema sababu nyingine inayochochea matukio hayo ni chuo kukosa uzio na hivyo kurahisisha mwingiliano wa watu na wanachuo.

Hivi karibuni wanachuo wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam waliandamana wakipinga kukithiri kwa vitendo vya wizi, ubakaji na ulawiti katika hosteli zao zilizoko Kigamboni.
source wavuti

No comments: