MATUKIO YALIYOJIRI TANZANIA 2012# karibu 2013



Ugonjwa wa Dk. Mwakyembe  Januari 3, 2012
HALI ya afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ilikuwa inasikitisha kwani licha ya kupata matibabu nchini India na kuendelea na tiba hiyo hapa nchini, hali yake haikuwa ya kuridhisha kutokana na kunyonyoka nywele, kope, ndevu na vinyweleo vyote.

Madaktari 229 wafukuzwa Muhimbili Januari 6, 2012
UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) uliwafukuza kazi madaktari 229 waliokuwa katika mafunzo kwa njia ya vitendo kutokana na mgomo wa siku nne wakishinikiza kulipwa posho zao za mwezi mmoja.

Umeme bei juu Januari 14, 2012
WAKATI gharama za maisha kwa Watanzania wengi zikizidi kupanda kila siku, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), iliidhinisha ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kwa Tanzania Bara na asilimia 28.21 kwa Zanzibar kuanzia Januari 15, 2012.
Madaktari waanza mgomo nchi nzima Januari 23, 2012
JUMUIYA ya Madaktari Nchini, ilianza mgomo nchi nzima hadi pale ambapo serikali ingeliridhia kulipa madai yao ndipo madaktari wangelirudi kuendelea na kazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Madaktari, Dk. Ulimboka Stephen, alisema mgomo huo ungelikuwa wa nchi nzima kwa madaktari kutotoa huduma.



Wanafunzi wanane wafa maji Arusha Februari 28, 2012
WANAFUNZI wanane kati ya kumi wa Shule ya Msingi Piyaya, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha, walifariki baada ya kusombwa na maji ya mafuriko ya Mto Radiru wakati wakitoka shuleni, jioni majira ya saa 11:30.

Mei 3, 2012 Watu saba wafa ajali ya basi la NBS
WATU saba walikufa papo hapo na wengine 54 walijeruhiwa baada ya basi la kampuni ya NBS lenye namba za usajili T 978 ATM lililokuwa likitokea Tabora kuelekea Arusha kupinduka katika eneo la Jineri, nje kidogo ya mji wa Igunga.

Dk. Ulimboka atekwa na kupigwa Juni 28, 2012
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika msitu wa pande, nje kidogo ya jiji Dar es Salaam.


Serikali yawashtaki madaktari Julai 7, 2012
SERIKALI iliwashtaki katika Baraza la Madaktari Tanzania, madaktari wanafunzi wa vitendo walioshiriki kwenye mgomo wa madaktari uliofanyika nchini kwa tuhuma za kuhatarisha maisha ya wagonjwa na kukiuka maadili ya taaluma yao.

Meli ya Mv Skagit yazama Julai 18, 2012
Kisiwa cha Zanzibar kilikumbwa na msiba mzito kutokana na kuzama kwa meli ya MV Skagit, mali ya Kampuni ya Seagull, iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam ikiwa na abiria wanaokadiriwa kuwa 290 pamoja na mizigo kuelekea Unguja, visiwani Zanzibar majira ya saa saba mchana. Watu 63 walifariki, 146 wakiokolewa hai na 81 hawakupatikana.


Sheria ya mifuko ya jamii moto Julai 27, 2012
VUGUVUGU la kupinga mabadiliko ya sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012 lilichukua sura mpya baada ya wabunge kutaka kuifanyia marekebisho mengine kwa sababu mwanachama hataruhusiwa kuchukua mafao yake kwa sababu yoyote mpaka hapo atakapofikisha miaka 55 au 60.

Ugonjwa wa ebola waingia nchini Agosti 5, 2012
UGONJWA hatari wa ebola ambao umeua idadi kubwa ya watu nchini Uganda uliripotiwa kuingia nchini katika wilaya ya Kyerwa, kijiji cha Bulongo, mkoani Kagera, ambapo mtoto wa miaka sita alionekana na dalili hizo.

Walimu watishia kuing’oa CCM Agosti 6, 2012
WALIMU walipokubali kurejea kazini na kuendelea kutafakari amri ya mahakama, mkakati mzito ulipangwa kuhakikisha hawakiungi mkono Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Mauaji ya Daudi MWANGOSI Septemba 3, 2012
Jeshi la Polisi lilimuua mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyekuwa anaripoti habari za ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani hapa.
Mwangosi alidaiwa kuuawa kwa bomu lililorushwa na polisi waliotaka kuizuia CHADEMA kufungua tawi katika kijiji cha Nyololo.

Waislamu waandamana Dar Septemba 21, 2012
MAELFU ya waumini wa dini ya Kiislamu waliandamana na kukusanyika kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam ambako walitoa tamko dhidi ya wanaoshambulia na kunyanyasa Uislamu, hasa kwa Marekani kutengeneza filamu ikimkashifu Mtume Muhammad (SAW).

Ajali yaua 10 Mbeya, mbunge anusurika Oktoba 3, 2012
MBUNGE wa Viti Maalum Mbeya kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, alinusurika kufa katika ajali iliyogharimu maisha ya watu takriban 10.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Mbalizi, wilaya ya Mbeya Vijijini. Gari la mbunge huyo liligongwa na kuteketea kwa moto papo hapo.

Kizaazaa cha mafuta Dar Oktoba 3 2012                     
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) baada ya kushusha bei za mafuta ya petroli na dizeli nchini, baadhi ya wafanyabiashara walizua kizaazaa kwa kuweka mgomo baridi wa kuuza mafuta hayo.



 Waislamu wachoma, wavunja makanisa Oktoba 12, 2012
KUNDI kubwa la Waislamu wenye imani kali, lilizusha vurugu kubwa zilizoambatana na kuchomwa moto na kuharibiwa makanisa manne huko Mbagala jijini Dar es Salaam, katika kile kilichoelezwa kuchukizwa na kitendo cha kijana mmoja wa Kikristo aliyedaiwa kukimwagia haja ndogo kitabu kitakatifu cha Kurani.

Ponda akamatwa kwa uchochezi Oktoba 17, 2012
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilimtia mbaroni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa, akikabiliwa na tuhuma mbalimbali za uchochezi.









Padri apigwa risasi Zanzibar Desemba 26, 2012
PADRI wa Kanisa Katoliki lililoko Mpendae visiwani Zanzibar, Ambrose Mkenda, alijeruhiwa kwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni  wakati akitoka kanisani.

No comments: