UHURU WA HABARI TANZANIA #Hekaya za Ray Mtani

Na Raymond Mtani
Leo ni siku ya uhuru wa habari dudiniani, lengo kuu la maadhimisho ya siku hii may 3, (world press freedom day) ni:

• kukuza uelewa kuhusu umuhimu wa uhuru wa habari na
• kukumbusha serikari wajibu wake wa kuheshimu na kuthamini haki ya uhuru wa kujieleza kama unavyotajwa katika Ibara ya 19 ya mkataba wa haki za binadam.

Labda kwa faida ya jumla Ibara ya 19 ya mkataba wa kimataifa wa haki za binaadam inasomeka hivi “Everyone has the right to freedom of opinion and expression; the right includes freedom to hold opinions without interference and to seek, receive and impart information and ideas through any media regardless of frontiers”

Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka. Zaidi tafsiri ya Ibara hiyo imehuishwa katika ibara ya 18 ya katiba ya JMT 1977 na mabadiliko yake ya mwaka 2005.
Kwangu mimi siku hiyo ni zaidi ya muhimu kwa ustawi wa demeokrasia ya nchi yetu, ni muhimu kwa ajili ya kuhamasisha na kuchochea mawazo mbadala, hasa ikizingatiwa kuwa mwaka huu waandishi na jamii ya wapenda haki za binadamu wanaadhimisha siku hiyo kukiwa na kumbukumbu ya matukio mabaya kupata kutokea katika historia ya nchi yetu,

Naam nitataja machache, mosi ni mauaji ya kinyama ya mwandishi Daudi mwangosi akiwa kazi kutafuta habari kama ibara ya 18,(b) ya katiba ya JMT inavyompa haki hiyo. Ipo kumbukumbu ya Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri kutekwa, kuteswa, kung’olewa kucha, jicho na kasha kutelekezwa hadi leo hii yungali anauguza majeraha huko Afrika kusini.

Vile vile tunaadhimisha siku hiyo kukiwa na kumbukumbu ya kutekwa, kuteswa, kungolewa kucha, meno na kutelekezwa katika msitu wa Pande kwa mwanyekiti wa jumuhiya ya mdaktari nchini Dr steven Olimboka, huyu alikuwa katika harakati za kukuza uhuru wa kujileza(haki ya msingi ya kikatiba)

Kama hiyo haitoshi ni hivi juzi may 1, mkuu wa mkoa wa Arusha alitishia waandishi wa habari akiwataka kuwa makini pindi wanapoandika habari zinazohusu migogoro ya viongozi akienda mbali zaidi na kudai roho zao zitakua mkononi

"Unapoingia katika mkakati wa kudhalilisha kiongozi wa serikali unakuwa umeiweka roho yako rehani, kuweni makini" alisema Magesa Mulongo mkuu wa mkoa wa Arusha katika maadhimisho ya siku ya wafanya kazi duniani.

Tunaadhimisha siku hii kukiwa na jaribio la Bunge kuzuia vyombo vya habari kurusha matangazo yake ya moja kwa moja ingawa jaribio hilo linaonekana kushidwa juhudi zingali zinafanywa hii ni kutokana na kiongozi mkuu wa bunge Speaker Anne Makinda kurudia mara kwa mara kuwa hawafanyi kazi taarifa za vyombo vya habari.

Mbali na msululu wa sharia mbovu zinazonyima waandishi na vyombo vya habari kwa ujumla kufanya kazi zao kwa weledi kwa kutoa taarifa zenye ushahidi wa kina, serikali imekuwa ikitumia lungu la sharia hizo mbovu kushitaki waandishi na kufungia kila chombo cha habari kinachokinzana na matakwa yake, wote tunakumbuka tukio la kufungiwa kwa gazeti la MWANAHALISI.

Orodha ni ndefu sana, yatosha kusema kila mtanzania kwa nafasi yake anawajibika kushinikiza serikali hii kuheshimu uhuru wa habari, kujieleza ni haki pekee ya msingi, siyo matakwa ya mtu bila kuwa makini kupitia haki hii tutaibiwa, tutanyanyaswa, tutateswa na kufanyiwa kila hila.
Namaliza kwa kusema ni rahisi sana kumuua mtu kuliko kumyamazisha kusema.

Kinabo mhitimu SUA aliejiajiri katika ufugaji wa samaki

Mawazo ya wahitimu wengi wa vyuo vikuu nchini katika miaka ya karibuni  imekuwa ni namna ya kupata  ajira zenye tija. 
Ndoto ya wengi ni kupata kazi za kipato kizuri na ambazo zitawawezesha kuishi vizuri, kumiliki gari, kujenga nyumba na mambo mengine lukuki.
Hata hivyo, baadhi wamekumbana na tatizo la ajira ambalo limewasukuma katika kubuni miradi ambayo  itawawezesha kumudu maisha na changamoto zake.

Mmoja wao, Simon Kinabo, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kilichoko Morogoro ameamua kujiajiri baada ya  kubuni mradi wa  ufugaji wa samaki.
Mradi huo  unaoitwa Rombo Unique Aquaculture, upo kilomita 60 kutoka mjini Moshi na kilomita nne kutoka makao makuu ya Wilaya ya Rombo, eneo la Mkuu.
Anasema akiwa mwanafunzi katika chuo hicho, akisomea Shahada ya Sayansi ya Viumbe wa Majini (BSc Aquaculture) alihamasika na somo la uzalishaji wa samaki na ndipo akaamua kuanzisha mradi huo kwa mtaji wake.
“Katika fedha zile za mkopo,  kila nikipewa na Serikali, nilichukua kiasi kidogo na kuanzisha nyumbani mradi wa kufuga samaki.
Niliamini ni mradi mzuri ambao unaweza kubadili maisha yangu,” anasema.
Anaongeza kuwa alianzisha mradi huo  kwa kuchimba bwawa dogo na kuanza kuzalisha samaki, kwa lengo la kuja kuwauza baadaye.

Mkopo wa CRDB
Anasema akiwa mwaka wa pili SUA  alipata taarifa ya kuwapo mradi wa SUGECO unaoendeshwa na chuo hicho na CRDB ambao unalenga kuwawezesha wanafunzi wa elimu ya juu kuingia katika ujasiriamali.
“Baada ya kupata taarifa hizo nilijitokeza kuandika andiko la kuomba fedha na baada ya usaili, andiko langu lilipitishwa na chuo na CRDB,” anasema.
Anaongeza kuwa baada ya kupitishwa andiko lake, alipokea mkopo wa Sh20 milioni kwa ajili ya kuanzisha mradi.
Baada ya kupokea fedha, aliamua kupanua bwawa  hilo na pia kuliongezea mifumo ya kuingiza maji kutoka Mto Ngwasi na kutoamaji ili liwe la kisasa.
“Nilinunua mabomba 100 ya futi 2,000 na sasa bwawa langu lina urefu chini, mita  tatu hadi sita na upana mita 30,” anaeleza.
Anasema kuwa baada ya upanuzi wa bwawa alinunua samaki wadogo 3,000 kutoka Gereza la Karanga mjini Moshi ambao walikuwa ni  wa jamii ya perege na kambare.
Anaongeza kuwa  kila kifaranga cha samaki alikinunua kwa Sh300 na kwamba hiyo ilikuwa Mei 5, mwaka  jana, alipoanza kuwapandikiza bwawani mwake.

Mafanikio ya mradi
Hadi sasa, Kinabo anasema bwawa lake linao  zaidi ya samaki  40,000, kati ya hao wakubwa ni 10,000 na wadogo 30,000.
Anasema , Juni mwaka huu  anatarajia kuanza kuvua samaki na  matarajio yake  ni kuvua tani  nne  za samaki.
“Nina imani tani hizo nne, nikivua naweza kupata zaidi ya Sh60 milioni na tayari nimepata masoko,” anasema  msomi huyo.
Anasema tayari, amefanya mazungumzo na wakuu wa shule kadhaa za sekondari  wilayani Rombo, Hospitali ya wilaya hiyo na maeneo kadhaa ambao wamekubali kununua samaki wake.
Kwa kutambua kuwa hawezi kufanya kazi  hizo peke yake, mjasiriamali huyo msomi amemwajiri mtunza mazingira, James Edmund,  pia hivi karibuni atakuwa na walinzi wawili na muuzaji wa samaki.

kwa hisani yamwanachi

Afrika ikatae kunyonywa na kugawanywa


Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  mwishoni mwa wiki limepitisha kwa kauli moja  Tamko la Kisiasa kuhusu Utatuzi wa  Migogoro  Barani Afrika kwa njia ya  Amani.
Tamko hilo  ambalo ndani yake  linaainsha  na kutambua mchango mkubwa wa   Muungano wa Nchi Huru za Afrika  (OAU) na sasa Muungano wa Afrika ( AU)  katika kuchagiza  na kusimamia  pamoja na mambo mengine, maendeleo ya nchi za Afrika na watu wake,  kupiga vita  umaskini, ujenzi wa utawala bora, demokrasia , haki za  binadamu na utatuzi wa migororo kwa njia za amani.

Kabla ya kupitishwa kwa Tamko hilo,  Baraza Kuu la Umoja wa  Mataifa,  kwa siku nzima ya Alhamisi na ijumaa asubuhi lilijikita katika  majadiliano  ya mada iliyohusu ‘utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani barani afrika’, ikiwa pia ni sehemu na  Baraza hilo kuadhimisha miaka  50   tangu kuanzishwa kwa OAU na baadaye AU.

Miongozi wa viongozi wakuu walioshirikia majadilaino hayo, na ambayo yaliandaliwa na Bw. Vuk Jeremic,   Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,   Rais wa  Equatoria Guinea Theodore Obiang Nguema Mbasogo, Rais Mstaafu wa Burundi Jean Pierre Buyoya  ambaye pia     Mwakilishi  maalum wa Muungano wa Afrika  huko Mali na Sahel,  wakiwamo pia mawaziri  kadhaa wa  Mambo ya Nchi za Nje.

Akiungana na wazungumzaji wengine katika mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi, pamoja na kuainisha sababu na vyanzo vya migogoro Barani Afrika, alisema, Afrika lazima ifikie mahali ikatae kugawanywa.
“Bara la Afrika lina fursa  nyingi,  Afrika inapanda chati. Afrika lazima ikatae kugawanywa, ikatae kudharauliwa na ikatae  kunyonywa” akasema Mwakilishi wa Kudumu, Tuvako Manongi.

Na kubainisha kwamba,  Afrika lazima pia ikatae kutambuliwa kama bara ambalo limejaa migogoro  . “  Huu ni wakati wa  kufufua  upya pan africanism,  hiki ni kipindi cha mwamko mpya wa Afrika. Lazima tufanye kazi kwa pamoja  ili kuwapa matumaini watu wetu” akasisitiza Manongi.

Wakati tukisherehekea maadhimisho ya miaka 50 wa OAU,  ni  vema kila mmoja wetu akaahidi  upya  kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na
Muungano wa Afrika  kama ilivyoainishwa  katika  Sura ya Saba ya Katima ya Umoja  wa Mataifa.

Akatoa mfano kwa kusema  uhusiano huo unapashwa kuendelezwa katika nyanja zote za  usalama na  maendeleo.  Kama ambavyo imeshashuhudiwa  katika   uundwaji wa Jeshi la  Mseto  kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika   katika Jimbo la Darfur ( UNAMID),  Misheni ya  Muungano wa Afrika huko Somalia, (AMISOM0  na tukio la hivi karibuni la kurejewa na  kuongozewa uwezo mpya Misheni ya Kutuliza Amani katika DRC ( MONUSCO) kulikoendana na kuridhiwa  upelekaji wa Brigedi Maalum inayoundwa na wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi.

Aidha akasema majadiliano hayo  ya Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa, yamefanyika ikiwa  ni siku chache tu,   tangu kufanyika kwa Mkutano wa Baraza la Usalama la Afrika katika ngazi ya Mawaziri nchini Tanzania,  mkutano ambao pia ulijadili kwa kina pamoja na mambo mengine  hali ya usalama  barani afrika , vyanzo vya migogoro na ufumbuzi wake.
Karibu wazungumzaji wote wakiwamo wawakilishi wa Marekani na Jumuiya ya Ulaya waliochangia majadialiano hayo ya utanzuaji wa migogoro kwa njia ya amani, licha ya  kutambua, kusifu na kupongeza kazi kubwa ambayo imefanywa na inaendelea kufanywa na   Muungano wa  Afrika na Taasisi za Kikanda katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, walisisitiza haja na  umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendeleza ushirikiano wake na Muungano wa Afrika.

Aidha wazungumzaji huo walitambua na kukiri kwamba  Bara la Afrika licha ya  changamoto mbalimbali zikiwamo za migogoro inayoibuka hapa na pale,  imepiga hatua kuubwa za kimaendeleo, kiuchumi na kijamii na kwamba   Bara hilo linastahili kupongezwa na kuendelea kusaidiwa.

Arudi shule baada ya utafiti wa TAMWA




UTAFITI wa kihabari uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Machi 2012 umefanikisha kumrudisha shuleni mwanafunzi wa sekondari aliyekuwa ametelekezwa yeye pamoja na familia yao.

Mwenjuma Magalu ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Komnyang'anyo alitelekezwa na babayake yeye pamoja na mamayake mwaka jana, hivyo kushindwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo licha ya kuchanguliwa kuendelea na masomo.

Hata hivyo baada ya utafiti wa kihabari kufanyika kijijini Msasa Wilaya ya Handeni na taarifa za mtoto huyo kushindwa kujiunga na sekondari baada ya mamayake (kwa sasa marehemu) kukosa uwezo kuripotiwa, alijitokeza mfadhili wa kumsomesha ambaye anagharamia masomo yake hadi sasa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi akiwa shuleni Komnyang'anyo, mwanafunzi huyo aliishukuru TAMWA kwa kuibua tatizo la familia yao kwa umma na kupatikana kwa mfadhili ambaye amemrudisha masomoni licha ya familia yao kutelekezwa.

"Binafsi nawashukuru sana hao (TAMWA) waliopaza sauti hadi mjuu wangu kurudi shuleni...hii kwetu ilikuwa ni ndoto kwetu maana mtoto mwenyewe alikuwa amekata tamaa kabisa kurudi shuleni na alikuwa kaanza kufanya vibarua mitaani huku wenzake wakiendelea na shule," alisema bibi wa mtoto huyo, Amina Mohamed akizungumza.

Bibi huyo akizungumzia maisha ya sasa ya familia hiyo alisema bado wanahitaji msaada wa huduma hasa baada ya mwanaye kufariki dunia mwaka jana na kumuachia watoto wake.

Aliongeza kwa sasa yeye ni mgonjwa wa TB anayetumia dawa hivyo kwa hali yake ameshauriwa kupumzika jambo ambalo limempa mzigo mkubwa kimajukumu mwanafunzi (Mwenjuma), kufanya kazi za nymbani kama kupika kulima na shughuli nyingine.


Hata hivyo mama wa mtoto huyo (Hadija Magalu) ambaye alitelekezwa na mzazi mwenzake alifariki dunia mwaka jana kwa tatizo la uzazi na kuiacha tena familia hiyo ya watoto watatu katika hali ngumu zaidi chini ya malezi ya bibi mzaa mama.

kwa hisani ya mjengwablog